Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ (ONMM 2024)

Zaburi 91

Read Scripture freely. Divine Threads study for this chapter is coming later.

1Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana, atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.
2Nitasema kumhusu Mwenyezi Mungu, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ninayemtumaini.”
3Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji, na maradhi ya kuambukiza ya kuua.
4Atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mabawa yake utapata kimbilio, uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.
5Hutaogopa vitisho vya usiku, wala mshale urukao mchana,
6wala maradhi ya kuambukiza yanayonyemelea gizani, wala tauni iharibuyo adhuhuri.
7Ijapo watu elfu wataangukia kando yako, kumi elfu mkono wako wa kuume, lakini haitakukaribia wewe.
8Utatazama tu kwa macho yako na kuona adhabu ya waovu.
9Ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako; naam, Mwenyezi Mungu ambaye ni kimbilio langu;
10basi hakuna madhara yatakayokupata wewe, hakuna maafa yatalikaribia hema lako.
11Kwa kuwa atawaagiza malaika wake kwa ajili yako, wakulinde katika njia zako zote.
12Watakuchukua mikononi mwao, ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.
13Utawakanyaga simba na nyoka wakali, simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu.
14Mwenyezi Mungu asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa; nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.
15Ataniita, nami nitamjibu; nitakuwa pamoja naye katika taabu, nitamwokoa na kumheshimu.
16Kwa siku nyingi nitamshibisha na kumwonesha wokovu wangu.”