Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ (ONMM 2024)

Zaburi 81

Read Scripture freely. Divine Threads study for this chapter is coming later.

1Mwimbieni kwa furaha, Mungu aliye nguvu yetu; mpigieni kelele za shangwe Mungu wa Yakobo!
2Anzeni wimbo, pigeni matari, pigeni kinubi na zeze kwa sauti nzuri.
3Pigeni baragumu za pembe za kondoo dume wakati wa Mwandamo wa Mwezi, na wakati wa mwezi mpevu, katika siku ya Sikukuu yetu;
4hii ni amri kwa Israeli, agizo la Mungu wa Yakobo.
5Aliiweka iwe kama sheria kwa Yusufu alipotoka dhidi ya Misri, huko tulikosikia lugha ambayo hatukuielewa.
6Asema, “Nimeondoa mzigo mabegani mwao; mikono yao iliwekwa huru kutoka kwa kikapu.
7Katika shida yako uliniita nami nikakuokoa, nilikujibu katika mawingu yenye ngurumo; nilikujaribu katika maji ya Meriba.
8“Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya: laiti kama mngenisikiliza, ee Israeli!
9Hamtakuwa na mungu mgeni miongoni mwenu; msimsujudie mungu wa kigeni.
10Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mungu wako, niliyekutoa nchi ya Misri. Panua sana kinywa chako nami nitakijaza.
11“Lakini watu wangu hawakunisikiliza; Israeli hakunitii.
12Basi niliwaacha katika ukaidi wa mioyo yao wafuate mashauri yao wenyewe.
13“Laiti watu wangu wangenisikiliza, laiti Israeli wangefuata njia zangu,
14ningewatiisha adui zao kwa haraka, na kuugeuza mkono wangu dhidi ya watesi wao!
15Wale wanaomchukia Mwenyezi Mungu wangejikunyata mbele zake, na adhabu yao ingedumu milele.
16Bali ninyi mngelishwa ngano iliyo bora, na kuwatosheleza kwa asali inayotoka kwenye mwamba.”