Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ (ONMM 2024)

Zaburi 138

Read Scripture freely. Divine Threads study for this chapter is coming later.

1Nitakusifu wewe, Ee Mwenyezi Mungu, kwa moyo wangu wote, mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako.
2Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, nami nitalisifu jina lako kwa ajili ya upendo wako na uaminifu, kwa maana umeitukuza ahadi yako zaidi ya jina lako.
3Nilipoita, ulinijibu; ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.
4Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Mwenyezi Mungu, wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako.
5Wao na waimbe kuhusu njia za Mwenyezi Mungu, kwa maana utukufu wa Mwenyezi Mungu ni mkuu.
6Ingawa Mwenyezi Mungu yuko juu, humwangalia mnyonge, bali mwenye kiburi yeye anamjua kutokea mbali.
7Nijapopita katikati ya shida, wewe unayahifadhi maisha yangu, unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, kwa mkono wako wa kuume unaniokoa.
8Mwenyezi Mungu atatimiza kusudi lake kwangu, Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako wadumu milele: usiziache kazi za mikono yako.